NAWASHUKURU KWA KUNICHAGUA KUWA MBUNGE WA B.A
GENERAL
Kila sifa njema
ni zake Allah (S.W) ambaye atakapo jambo
husema kuwa na likawa, Rehema na Amani zishuke juu ya kipenzi chake na chetu
pia Muhammad (s.a.w) na wafuasi wake wote.
Napenda kutumia
nafasi hii kuwashukuru wote walionipigia kura na wasionipigia kura.
Walionipigia kura ninawashukuru kwani wameonesha imani yao kwangu na wanaamini
kuwa ninaweza kukifanya kile watakachohitajia. Wasionipigia kura nao sinabudi
kuwashukuru kwani ni changamoto kwangu isije nikabweteka kwa kujiona kuwa
ninaweza kumbe ninatakiwa kuongeza juhudi ili niweze zaidi.
Mawakala wangu,
wagombea wenzangu na wote waliosimamia zoezi la uchaguzi nao siwezi kuwasahau
kwani walikuwa tayari kuhakikisha wanasimamia zoezi kwa hatua zote , namuomba
mwenyezi Mungu awalipe kila la kheri kwa uadilifu wao.
Ndugu zangu
nashukuru kwa kuniamini kwenu na kunipa dhamana kubwa, dhama mliyonipa
nitajitahidi kadri ya uwezo wangu kuhakikisha ninaifanya kwa nguvu zangu zote,
lakini kikubwa ninachowaombeni ni dua zenu kwani bila msada wa Mwenyezi Mungu
siwezi kufanya lolote lile.
Pia litakuwa si
jambo la kiungwana kama nitawasahau kuwashukuru wale ambao hawajapiga kura na
wale walioharibu kura zao. Makundi haya mawili ninaamini wapo waliochukua
maamuzi yao kutokana na fikra, imani na mitazamo yao, lakini wapo waliosukumwa
na marafiki. Hawa waliosukumwa na marafiki tunaweza kusema wanafanya mambo
KIBUBUSA yaani wanafuata mkumbo. Kufanya jambo KIBUBUSA kwa msomi tena wa chuo
kikuu ni jambo linaloweza kushangaza jamii, kwani jamii inaamini kuwa msomi
ndio kiigizo chema na ni chanzo cha fikra na maamuzi sahihi. Hapa tatizo si
maamuzi bali tatizo ni kufanya jambo kwa kufuata maamuzi ya mtu fulani pasina ya kujua kuwa wewe mwenyewe unatakiwa
uwe na sababu, fikra, mtazamo, haja na uwe ndio chanzo cha maamuzi.
Katika tasinia
ya siasa kuchafuana na kupakana matope limekuwa ni jambo linaloonekana kuwa ni
la kawaida. Nasi katika mchakato wetu wa uchaguzi wapo walioeneza sifa zisizo
zangu wengine walinichafua ili nikataliwe. Hawa wote sinabudi kuwashukuru kwani
maneno na mapambo yao yalikuwa ni ufunguo wa kuwafanya wapiga kura wafanye
udadisi juu yangu na kupata ukweli na hatimaye wakafanya maamuzi sahihi.
Muda hautoshi na
nafasi ni ndogo wako wengi wakushukuriwa kikubwa niseme tu kila mmoja kwa
nafasi yake ninamshukuru, na ninaendelea kuwaombeni mniombee kwa Allah ili
niweze kufanya kile kinachomridhisha yeye na kile ambacho ninyi pia kitawaridhisha
kumbukeni kuwa “HAYA TULIYONAYO NDIO
MAISHA YENYEWE, HAKUNA MAISHA MENGINE ZAIDI YA HAYA KWA HAPA DUNIANI.
Kiongozi ni kama
KIRAKA katika nguo. Kiongozi makini ni kama KIRAKA katika nguo iliotoboka na
kiongozi mbovu ni kama KIRAKA katika nguo isiyotoboka. KIRAKA katika nguo
iliyotoboka kina kazi ya kufanya, nayo ni kusitiri sehemu iliyowazi na KIRAKA
katika nguo isiyotoboka hakina kazi ya kufanya ingawa utaniambia ni pambo.
Tangu enzi za wahenga hadi leo KIRAKA hutumika kwa kuziba sehemu iliyowazi na
wala si pambo kama usemavyo wewe. Ni matumaini yangu kuwa wote tuliochaguliwa
kwa kushirikiana nanyi mliotuchagua kwa msaada wake Allah tutafanya mambo
yatakayo tuwezesha kupata mafanikio hapa Duniani na kesho Akhera.
Ndimi: FAKIHI
S. MSHAMU (MWL/Dr. NAHONYO)