Friday, December 14, 2012


BISMILLAHIR RAHMAANIR RAHIIM

HUKUMU MBALIMBALI ZINAZOHUSIANA NA MWANAMKE WA KIISLAMU

MIPAKA YA KUJIPAMBA, KUJIPODOA NA KUJIREMBA KWA WANAWAKE KATIKA UISLAMU.

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
UTANGULIZI.

Uislamu ni dini iliyomuwekea mwanadamu mipaka kimwili, kiakili na kiroho. Miongoni mwa mipaka ya akili ni pamoja na kupewa ruksa ya kutafakari viumbe mbalimbali lakini ikakatazwa kufikiri na kutafakari juu ya dhati ya Muumba na kaifia yake. Mwili nao umewekewa mipaka mbalimbali. Suala la mwanamke kujipamba ni suala la kimaumbile ambalo mwanamke hulelewa katika hali hiyo ya kupambwa, kama Allah alivyosema ndani ya Qur’an (43:17). Nafsi ya mwanamume nayo imeumbwa na sifa ya kupenda, kutamani na kuvutiwa na mapambo akiwemo mwanamke (3:14). Hivyo Uislamu haujakaa kimya juu ya suala la mapambo ya wanawake bali umeliwekea mipaka na hukumu mbalimbali suala hilo. Mapambo ya wanawake yamegawanyika katika sehemu kuu mbili: sehemu ya kwanza ni yale ya kimwili ikiwemo ngozi na sehemu nyinginezo za mwili. Haya ni mapambo ya Asili na Sheria ya Kiislamu huyachukulia haya kuwa ni mapambo ya ndani au ya kimaumbile au “Ziinatun khaliqiyat”. Aina ya pili ya mapambo ni yale ya mavazi na vinginevyo vyenye kupambwa katika mwili mfano dhahabu n.k. Wanazuoni wengi wamezungumzia sana mapambo ya mavazi na dhahabu, lakini sijaona kama wamezungumzia sana suala la namna ya kuupamba mwili.

Katika makala hii tutazungumzia hukumu mbalimbali zinazomuhusu mwanamke, tukianza na mwili wake na suala zima la kujipamba.

NYWELE ZA KICHWA

Nikianza na nywele za mwanamke: Yako mambo kadhaa yanayohusiana na suala la nywele za mwanamke likiwemo suala la mwanamke kujipamba kwa kubadilisha rangi ya nywele zake ili ziwe nyeusi sana na mfano wa hivi. Pamoja na kuwa dhahiri ya jambo hili ni kuwaiga wanawake wa kikafiri ambapo mwanamke wa Kiislamu amekatazwa kisheria, si hivyo tu bali zimekuja hadithi mbalimbali zikikataza jambo hili hasa hasa kuzibadili nywele nyeupe kwa kuziwekea madawa na kemikali  ili ziwe nyeusi kuliko zilivyo katika asili yake. Na uharamu unakuwa mkubwa zaidi pale ambapo ubadilishaji wa nywele hizo unapoambatana na madhara ya kiafya kama vile matumizi ya kemikali zenye kunyonyoa nywele au hata kuathiri kichwa hadi ubongo kama kalikiti inavyofanya nywele kuwa kama majani yaliyotafunwa yakamezwa kisha yakatapikwa “Kaasfin Maakuul” ! Utumiaji wa madawa ya nywele unaleta madhara kwa mwenye kuwekewa na mwenye kuweka. Hali hii inayafanya yawe hayafai kisheria kwa msingi muhimu wa Sheria: “Haifai kudhuru wala kulipana madhara.” [Ibn Maajah na ad-Daaraqutniy].
Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: {Wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamizo} [Al-Baqarah 2: 195].  Na pia amesema; {Wala msijiue} [An-Nisaa 4: 29].
Imethibitika kitiba kuwa baadhi ya madawa ya nywele yana kemikali zinazoleta madhara makubwa sana kwa wanawake. Kwa mfano madawa yenye madini ya Zebaki au “Mercury” ni sababu kubwa miongoni mwa sababu zinazoleta uvimbe au “fibroids” katika kizazi kwa wanawake wengi. Hata maumivu makali wakati wa hedhi au dysmenorrhea pamoja na mabadiliko ya mfumo wa mwanamke kupata hedhi huwa pia yanasabishwa nayo. Hivyo Uislamu unachunga maslahi ya mwanadamu na hautaki awe ni mwenye kudhurika.
N.B: Inaruhusiwa kwa mwanamke kutumia mafuta mazuri ya nywele yasiyo na madhara kwa nywele na ngozi ya kichwa chake na wala hayabadilishi rangi ya nywele bali yanachofanya ni kuzilainisha na kuzifanya zipendeze pamoja na kuwa rahisi kuzichana. Bali hili ni miongoni mwa matendo ya kimaumbile yanayojulikana kama “Sunanul Fitra”

Jingine linaloambatana na nywele ni suala la kusukia nywele za bandi na hili ni haramu katika hali zote hasahasa pale ambapo nywele za mwanamke ni fupi naye anataka kuzifanya ziwe ndefu au anataka kujizidishia urembo kwa kuongeza nywele za bandia; basi msusi na msukwaji wanalaniwa na Allah! Tunasimuliwa kisa cha mwanamke wa Ki-Answaariy aliyemuozesha binti yake ambaye nywele zake zilianza kunyonyoka. Mwanamke huyo wa Ki-Answaariy alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumtajia kwamba "Mumewe (mume wa mwanangu) ameona kwamba nimwachie avae nywele za bandia" Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Usifanye hivyo kwani Allaah Huteremsha laana Yake kwa wanawake kama hao wanaoongeza nywele za bandia)” [Al-Bukhaariy 7:133, kutoka kwa Mama wa Waumini 'Aaishah Radhiya Allaahu 'anha]. Katika Riwaya nyingine imepokewa kwa Asmaa’ (Radhiya Allaahuanha) kwamba mwanamke fulani alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Ee Mtume wa Allaah! Binti yangu amepatwa na surua zikapukutika nywele zake, nami nimemuozesha; Je, niziunganishe?” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamjibu: “Allaah Amemlaani mwenye kuunganisha nywele zake (au nywele za mwengine kwa nywele nyengine) na mwenye kuungwa (au kuvaa nywele hizo)” [Al-Bukhaariy, Muslim na an-Nasaaiy]. Na katika riwaya nyengine: “Mwenye kuunganisha nywele na mwenye kumtaka mwengine amfanyie kazi hiyo (mwenye kutamani kuzivaa nywele hizo za bandia)”.
Pia imepokewa kwa Humayd bin ‘Abdir-Rahmaan kuwa alimsikia Mu‘awiyah (Radhiya Allaahuanhuma), mwaka wa Hijjah, akiwa juu ya mimbari, akiwa ameshika nywele zilizokatwa katika mikono ya Harasiy (Mtoto wa Amiri), akasema: “Enyi watu wa Madinah! Wako wapi wanazuoni wenu? Nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akikataza tabia hii (nywele za bandia) na alikuwa akisema: ‘Hakika walihiliki Bani Israili pale wake zao walipoichukua tabia hii (ya kuunganisha nywele)’” [Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaaiy].
Wengine siku hizi hufikia kuweka mabanio makubwa (help me) ili waonekane nao wanazo! Hili Sheria inaweza kulizungumzia kuwa watalipwa kwa nia zao, na kuwa mwenye kuwadanganya waislamu si katika wao. Hili linataka kufanana kidogo na jawabu alilotoa Shekhe Ibn Baaz alipoulizwa kuhusiana na hukumu ya mwanamke kuvaa viatu venye soli ndefu sana. Shekhe alisema kuwa jambo hili halipendezi Kisheria: kwanza; kwa sababu ni udanganyifu wa kutaka kuwaonyesha watu kuwa mvaaji ni mrefu wakati siyo mrefu, pili ni hatari kwa mwanamke kutokana na uwezekano wa kuanguka kirahisi na tatu ni jambo lenye madhara kiafya kama mara nyingi walivyowahi kusema madaktari.
Ama kuhusu mwanamke kupunguza nywele zake za kichwa hilo halina uharamu wowote japo haipendezi mwanamke kunyoa nywele ambazo kimsingi ni pambo lake kubwa hadi Sheria ikamruhusu kuondoa kwa kupunguza sehemu ndogo sana ya nywele zake wakati wa Hijja ambayo ni ibada tukufu sana. Hata hivyo kama ataamua kunyoa au kupunguza nywele zake sharti achunge mipaka ya Allah kwani ni haramu kwake kunyolewa na kinyozi mwanamume ambaye si maharim wake.

MWANAMKE MWENYE NDEVU.

Ndevu ni pambo la asili la wanaume. Si jambo la kawaida kibaiolojia mwanamke kuwa na ndevu!! Ndevu zinaweza kuharibu sura ya mwanamke au kumpelekea kufanana na wanaume. Ikiwa hali ndiyo hiyo hapo itaruhusiwa kisheria kwa mwanamke kuziondoa. Isipokuwa pale itakapoonekana kuwa kuzinyoa huko kunazifanya ziote na kukua zaidi, hapo ni bora kwake kutokuzinyoa.

 

KUTOA NYWELE ZA USONI NA ZA MWILINI

 

Ni hakika kuwa Uislamu unawaamuru wafuasi wake yaani Waislamu wawe ni wenye kuwa wasafi katika kila hali. Usafi na utohara ni miongoni mwa sifa za kipekee zinazopatikana kwa Uislamu. Hata katika jangwa la Makkah wakati ambao kulikuwa na uhaba wa maji Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Alimuamuru kipenzi Chake kwa kumwambia: {Na nguo zako uzisafishe} (74: 4).
Kwa ajili ya hiyo ndio Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuamuru kuwa tuwe ni wenye kunyoa nywele za makapwa na za kinena. Hivyo, ikiwa nywele za mwilini zitakuwa ni zenye kuleta uchafu au vigumu kuweka usafi basi zinaweza kunyolewa bila ya tatizo lolote. Nywele ambazo mwanamume hafai kunyoa ni ndevu zake. Hizo zinafaa zifugwe na kukirimiwa kwa kutunzwa.
Ama kuhusu kutoa nywele za mikono na miguu kwa mwanamke ni jambo linaloruhusiwa. Tofauti imekuja katika kutoa nywele za uso kwa mwanamke. Wanazuoni wa Hanbali wamesema: “Mwanamke ameruhusiwa kutoa nywele za uso, ikiwa kwa idhini ya mume kwani ni katika mapambo”. Imaam an-Nawawiy yeye amekataa hilo kwani kwake amechukulia kuwa kutoa nywele hizo ni sawa na kuchonga nyusi. Abu Daawuud yeye amesema kuwa kutoa nywele za uso hakuingii katika kukata nyusi.
Kule ambako kumekatazwa na Uislamu kama tulivyotangulia kusema ni kuchonga nyusi, kwani wenye kufanya hivyo wamelaaniwa kwa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pale aliposema: “Wamelaaniwa wanawake wenye kutoa nyusi na mwenye kutolewa” (Abu Daawuud kwa Isnadi iliyo nzuri). Naye atw-Twabariy ameeleza kuhusu mke wa Abu Ishaaq ya kuwa alikwenda kwa ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha), naye alikuwa ni mwanamke kijana mwenye kupenda uzuri, akamuuliza: “Mwanamke anatoa nywele za usoni kwa ajili ya mumewe”. ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) akajibu: “Jiondoshee yanayokukera kiasi unavyoweza” (Fat-hul Baariy).
Kwa hiyo, kunyoa nywele za mikono, miguu na uso inaruhusiwa lakini kunyoa nyusi, kuzichonga au kuzipunguza ni haraam.
KUNYOA NYUSI
Kutoka kwa 'Abdullahi bin Mas'uud (Radhiya Allahu 'anhu) kwamba: ((Allah Amewalaani watu wenye kuwachanja wenzao (tattoo) na wenye kuchanjwa, na wenye kuwanyoa wenzao nyusi na wenye kunyolewa na wenye kuchonga meno yao (kama kufanya mwanya) kwa ajili ya kujipamba kubadilisha maumbile ya Allah) [Al-Bukhaariy Hadiyth Namba 5948 na Muslim Namba 2125]
Wako  baadhi ya mashekhe wanaohalalisha suala hili la kunyoa nyusi, kwa  itikadi yao potofu au kwa kutokujua kwao, yaani mwanamke kunyofoa nyusi kwa ajili ya mumewe! Jambo hili ni haramu hata kama mwanamke ataamua kuvaa Niqaab, maadam ni jambo lililoharamishwa, hivyo haliwezi kuhalalika kwa vijisababu kama hivyo vya kumrembea mume au kuvaa Niqaab mwanamke akitoka n.k.

Hadiyth ifuatayo inatuonyesha wazi uharamu wake: Amesema Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu): “Allaah Amewalaani wenye kuchanja, na wenye kuchanjwa, na wenye kunyoa nyusi, na wenye kuchonga meno kwa urembo, na wenye kubadilisha umbile la Allaah. Akamuuliza yeye mwanamke kuhusu jambo hilo. Akamjibu kwa kusema: "Kwa nini nisimlaani yule aliyelaaniwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na aliyelaaniwa katika Kitabu cha Allaah. Amesema Allaah Aliyetukuka: 'Na anachokupeni Mtume chukueni, na anachokukatazeni jiepusheni nacho' (59: 7)" (Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa'iy na Ibn Maajah).
Imaam al-Haafidhw Zakiyyud-Diyn 'Abdul-'Adhwiym bin 'Abdil-Qawiyy al-Mundhiriy katika kitabu chake Tahdhiyb at-Targhiyb wat Tarhiyb minal Ahaadith asw-Swihaah, uk. 353–354 anatueleza faida ya Hadiyth iliyoinukuliwa hapo juu kwa kusema: “Kuharamishwa kuungwa nywele, kuchonga meno, wenye kuchanja, kuchonga nyusi na matendo ya kujipamba ambayo yanakaza ngozi na kukataza kutokeza kwa mikunjo na miaka kusonga. Hekima ya kuharamishwa haya yote ni kule kubadilisha maumbile ya Allaah na kutoa picha ya ughushi, udanganyifu na uongo. Yanapodhihiri mambo haya ya haramu katika jamii, ni dalili kubwa ya uharibifu, ubadhirifu dhahiri na kuipatia dunia umuhimu. Kila mara anapozidi mwanamke kukimbia nyuma ya umbo la uongo, ndipo anauendea haraka uzee, hivyo kupoteza uzuri wake na kuwa ajuza mapema".
Ni haramu vile vile kuondoa nyusi na kuweka nyusi za bandia juu yake pamoja na Kutoboa nyusi na kuweka kipini. Na haya mambo ya kutoboatoboa ambayo yanakatazwa kisheria kwa kuwa ni kuharibu maumbile yameenda hadi katika matumbo na ulimi. Hukumu hii inakwenda pia katika kope za kupandika. Haifai kufanya hivyo Kisheria.

Lakini ikiwa nyusi za mwanamke zimezidi kuwa nyingi hadi zikawa zinaning'inia na kufunika macho na kuleta taathira ya uonaji, inafaa kuzitoa sehemu hiyo inayosababisha tatizo.
Ama kuhusu nyusi kuungana, kuna ikhtilaaf za Maulaamaa, kuna wanaosema inafaa kuzinyoa kwa kuona kwamba hiyo si sehemu ya nyusi. Na kuna wanaokataza kwa kuwa wameona kwamba maadamu hazileti madhara ya uonaji hakuna sababu ya kuzitoa kwani kuzitoa ni kwa ajili ya kuleta uzuri.
Kutokana na ikhtilaaf hizo naona kwamba, ikiwa nyusi hizo za katikati zilizoungana zikiwa hazina madhara yoyote ni bora kuziacha, na huenda utakapoanza kuzinyoa ukafikia kuzinyoa na hizo ambazo si za katikati na ukaingia kwenye laana zilizotajwa katika hadithi na pia ukashawishika kwa kuzinyoa hizo, ukawa unafikia kuzitengeneza na nyusi zako za kawaida kwa kuhisi kunakupendeza na hivyo ukawa umeshatumbukia kwenye makatazo na madhambi.

KUWEKA DAWA NYWELE ILI KUZIFANYA ZIPENDEZE
Sheria ya kutia rangi nywele ni kwa yule mwenye mvi katika kichwa. Hili ni katika mapambo yanayofaa kisheria.  
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwakataza Waislamu kuigiza watu wengine na kufuata nyendo zao, ili wawe daima kinyume na kutambulikaa na mambo yao. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) anasimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika Mayahudi na Manasara hawatii rangi mvi zao basi nendeni kinyume nao” (al-Bukhaariy).
Amri hii si lazima ni kwa wenye kutaka kama inavyodhihirisha matendo ya Maswahaba. Abu Bakr na ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) walikuwa wakitia rangi nywele zao na ‘Aliy, Ubay bin Ka‘b na Anas (Radhiya Allaahu ‘anhum) walikuwa hawatii.
Ama kuhusiana na rangi inayofaa kwa mtu kupaka kwa mzee mkongwe, ambaye kichwa chake kimejaa mvi, ni rangi nyekundu na haifai kutumia rangi nyeusi. Ndio maana siku alipokuwa Abu Bakar (Radhiya Allaahu ‘anhu) wakati ilipotekwa Makkah huku amembeba baba yake, Abu Quhaafah (Radhiya Allaahu ‘anhu) mpaka akamweka mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akaona kichwa chake kilivyojaa mvi alisema: “Badilisheni hizi mvi lakini msimtumie nyeusi” (Muslim).
Baadhi ya Maswahaba walikuwa wakitumia katumu ambao ni aina ya mmea kutoka Yemen unaotoa rangi nyekundu iliyowiva na kukoza sana au hina ambayo ni rangi nyekundu.
Rangi na hina au katumu zinafanana kwa kuwa zote zinabadilisha rangi ya nywele na hata umbile lake la kawaida. Lakini hakika ni kuwa rangi hii ya kemikali ina tofauti kubwa sana na hina kwani hii ya awali huwa inatiwa kemikali ambayo inaweza kuleta madhara. Kwa hiyo, ni juu yetu kutazama ile kanuni muhimu kuwa: “Chenye kumletea madhara mwanadamu huwa kwake ni haramu”. Ni bora kwetu kuachana na rangi hizo ila tu tunapoyakinisha kuwa hazina madhara kwetu.
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika Allaah Aliyetukuka ni Mzuri na Hakubali ila zuri” (Muslim). Kutia rangi nywele ni miongoni mwa mapambo ambayo imeruhusiwa kwa Muislamu kwa kubadilisha mvi na pia kuziweka nywele katika hali nzuri.
Kile ambacho hakiruhisiwi ni kwa mkongwe kutia rangi nyeusi au ikiwa kama zilivyo rangi za siku hizi kwa sababu ya kutengenezwa na kemikali zinakuwa na madhara. Pindi inapojulikana kuwa rangi hizo zina madhara basi inakuwa haifai kwa Muislamu kutumia. Na kwa hakika ni kidogo zisizokuwa na madhara kwa miili yetu.

KUJIPAKA CREAM KWA AJILI YA KUNG’ARISHA USO.

 

Ikiwa cream hiyo itakuwa haibadilishi rangi ya ngozi au haichubui bali inafanya tu uso uwe laini kisheria itakuwa inafaa. La sivyo kama ina madhara itakuwa ni haramu maana kila chenye madhara ni haramu.

 

 

KUPAKA WANJA

 

Mwanamke kupaka wanja inafaa na ni Sunnah lakini yapasa ampakie mume wake akiwa nyumbani kwake kwani wanja ni urembo na mapambo na hayo anayefaa kuyaona ni mume wake na si watu wengine huko nje. Hivyo, haifai kupaka wanja mwanamke akitoka nje kwani hayo ni mapambo na hayafai kuonwa na wasio Mahrim zako. Wanja pia ni dawa kwa magonjwa ya macho, hivyo kukiwa na dharura ya mwanamke au mwanamme kupaka kwa ajili ya kuondoa ugonjwa kutakuwa hakuna tatizo lakini sharti asijionyeshe. Tunaweza kulijumuisha hili na eye liner pamoja na eye shadow ikiwa zitakuwa ni kwa ajili ya mume wake tu. Lakini kama zitahusisha kutoa nyusi ndipo zipakwe zitakuwa haramu. Hata lipstick itakuwa katika hukumu hii hii, kuwa ni vitu vyenye kufaa kwa ajili ya mume tu. Lakini katika lipstick ikiwa itajulikana kuwa imetengenezwa na vitu vya haramu kama mafuta ya nguruwe itakuwa haifai japo ni kwa ajili ya mume. Yako mambo mengi yanayotia Shubha juu ya lipstick!


KUDUNGA AU KUTOBOA PUA, KUCHONGA MENO, KUTOBOA MASIKIO NA TUMBO NA KUTIA CHALE.

Uislamu umeruhusu mwanamke kutoboa masikio kwa ajili ya kutia kipuli na mapambo mengineo. Ama kwa tumbo, agizo ni, “Amewalaani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenye kuchanja – kutia chale (tattoo) na mwenye kuchanjwa, mwenye kuchonga meno na mwenye kuchongwa”. Qiyasi au kipimo ni kuwa ikiwa kuchanjwa kumekatazwa seuze kujitoboa mwili.

Hivyo, kujitoboa masikio ni miongoni mwa mapambo kwa wanawake yanayojulikana na yaliyokubaliwa na wanachuoni ilhali tumbo si pambo na kwa hiyo haifai. Hata hivyo haifai kwa mwanamke kutoboa sikio lote!

Shaykh ‘Abdullaah Jibriyn anasema, kutoboa tumbo ni katika mateso ya mtu binafsi, na si sehemu inayotumiwa kupambwa na hakuna manufaa yoyote kwa kitendo hicho, na isitoshe inaingia kwenye fungu la kubadilisha maumbile ya Allaah.

KUWEKA MENO YA DHAHABU
Meno ya dhahabu yanaweza kuwekwa na Muislamu kwa dharura inayokubalika kisheria. Hii ni kwa mujibu wa Hadiyth iliyosimuliwa na Arfajah bin As‘ad: Abdur-Rahmaan bin Tarafah alisema kuwa babu yake Arfajah ibn As‘ad (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikatwa pua yake katika vita vya Kilaab, hivyo akatia pua ya fedha, lakini ikaanza kunuka. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuamuru atie pua ya dhahabu (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy). Hadithi hii inatuonyesha jinsi Sheria yetu tukufu inavyotazama maslahi ya mwanadamu kwa kiwango kikubwa sana ili mwanadamu kama huyo asiwe ni mwenye kudhurika kwa chochote. Sheria ya Kiislamu imekwenda mbali zaidi kiasi cha kukipa ruhusa kitu ambacho ni haramu ili kusaidia kuleta nafuu kwa mwanadamu. Kwa hiyo, ikiwa ipo dharura ya kisheria kutia jino la dhahabu kutakuwa hapana shida yoyote ile.
KUJICHUBUA (MKOROGO)

Kujichubua ni jambo la haramu kwa mjibu wa sheria ya kiislamu kwani  jambo hilo ni katika kubadili sifa za maumbile aliyoumbiwa mwanadamu na Allah, kwa hapa tunamaanisha ngozi. Mwenye kujichubua ni kama vile hayuko radhi na maumbile aliyoumbiwa na Allah. Hali hii kama vile mwanamke anamkosoa Allah Muumbaji juu ya rangi ambayo kamzawadia ambayo pengine kulingana na maumbile yake ndiyo inayomfaa zaidi, pengine weupe anaoutaka ni madhara kwake na kwa afya yake. Tena tazama Muumba alivyo na hekima, ngozi nyeusi zinavumilia mionzi ya jua kuliko ngozi nyeupe! Hali hii imenasibiana na hali ya jua kali na joto katika nchi za kitropiki na bara la Afrika kwa upana wake, ambapo watu zaidi ya asilimia 90 ni watu weusi. Kwa hiyo kutafuta weupe kwenye Mekako na makopo mengine kunazidisha hatari yaw ewe mwanamke kupata magonjwa kama kansa ya ngozi. We dada mkorogo utakuua! Ni maneno ambayo mara nyingi husemwa kama kwa matani lakini yana ukweli ndani yake. Mkorogo unakufanya uwe chuichui! Uso mweupe vidole vyeusi ndio kazi ya mkorogo!!! Tena hatari inakuwa kubwa zaidi pale mwanamke anapomeza madawa tumboni lakini yanachubua ngozi! Hapa kuna hatari kubwa sana kwa ini na viungo vingine huko tumboni.


RANGI ZA KUCHA
Rangi ya kucha (Cutex) ni kitu ambacho kinazuia maji kufikia ngozi ya sehemu husika, kwa hivyo wudhuu wa mtu na Swalah ya mwenye kutia rangi ya kucha itakuwa haifai. Hivyo ikiwa mtu ataweka rangi ya kucha itampasa aitoe kila anapotaka kufanya wudhuu. Haya ni mashaka watakayojibebesha wanawake na kujikalifisha kwa jambo ambalo haliko katika ada za Kiislamu.
Wanawake wa Kiislamu ni bora kutumia hinna katika mapambo ya miili yao kuliko rangi za kucha kwani henna ni katika vipodozi vya Kiislamu na kutumia ni kufuata Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba zake hivyo ni kupata thawabu. Na bila ya shaka wenye kupaka rangi kucha watakuwa wamefuga kucha, jambo ambalo halipasi katika desturi zetu za Kiislamu kwani tumeamrishwa zisipindukie siku arubaini iwe tumeshazikata kama ilivyo dalili katika Hadiyth ifuatayo yenye kutaja mambo ya fitwrah (Maumbile ya asili 'Pure Nature of Creation').
Ama kuhusiana na kucha za bandia au za kubandika artificial), hizi hazifai kutumia maana ni kujifananisha na wasiokuwa waislamu.
Zamani tulipokuwa shule za Msingi kila siku tulikuwa tunakaguliwa na kukatwa kucha siku hizi mambo yamebadilika, usomi siku hizi ni mtu kuwa na kucha ndefu!!

DAWA ZA KUONGEZA MAKALIO, MAZIWA AU MCHINA (KWA KISWAHILI CHA LEO).

Hizi ni haramu moja kwa moja na haifai kwa mwanamke wa Kiislamun kutumia dawa hizi maana zina madhara makubwa kiafya.


UMUHIMU WA HADITHI YA MAMBO MATANO YA FITRA.

Usafi bora ni ule uliotajwa katika hadithi hii:  ((Imetoka kwa Abu Hurayrah kwamba Mtume kasema; ((Fitwrah ni tano, au (vitu) vitano ni miongoni mwa Fitwrah, Kutahiri (Circumcision), kunyoa (au kupunguza) nywele za sehemu ya siri (pubic hair), kukata kucha, kunyofoa (au kunyoa) nywele za kwapani, na kupunguza masharubu)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

((Imetoka kwa Anas bin Maalik ambaye alisema; Mtume alituwekea muda wa kupunguza masharubu, kukata kucha, kunyofoa (au kunyoa) nywele za kwapa, na kunyoa (au kupunguza) nywele za sehemu za siri (pubic hair), kwamba tusiziache zaidi ya siku Arubaini)) [Muslim, Abu Dawuud, At-Tirmidhiy na An-Nasaaiy]. Haifai kutumia Veet ambayo ni shaving cream kwani ina madhara kiafya.

Wako watu wanafuga kucha zikawa kama za paka. Kimsingi hali hii humfanya mtu asiweze kujitwaharisha vizuri, maana kwa mfano ili kujitwaharisha na janaba inatakiwa maji yaingie kila pahala. Upo uwezekano kuwa kuna watu wana janaba za miaka na miaka na wanaingia misikitini!!

Sheria inatuelekeza kuwa tunapokata nywele au kucha tuzifukie. Hii ni kanuni ya kutunza mazingira katika Uislamu. Vile vile inaweza kukuepusha na uchawi maana kuna watu huchukua kucha na nywele katika kuroga kwao. Ikiwa ni vigumu kuzifukia chini basi ni bora kuzichoma au kutumia utaratibu utakaofanya ziteketee. Ni jambo baya katika Uislamu na lenye kukera sana mwanamke kutupa ovyo nywele zake. Wengine hufikia hata kutupa ovyo pedi zilizotumika. Uislamu unatukataza kujidhuru na kuwadhuru wengine. Itakuwaje uachi pedi zako bafuni au chooni ziwe zinawakera wengine. Unapata madhambi makubwa dada yangu. Jirekebishe


KUTUMIA KUNGUMANGA

Kungu manga hazifai kutumia katika Uislamu kwa kuwa zinalewesha na katika Uislamu kila kinacholewesha ni pombe na kila pombe ni haramu.

KUKATA KUCHA NA NYWELE WAKATI WA HEDHI

Wanawake wengi wanayo dhana au wanaamini kuwa wakati mwanamke akiwa katika siku zake na viungo vyake vyote vinakuwa si tohara jambo ambalo si sahihi. Mtume Swalla LLahu ‘Alayhi Wasallama siku moja akiwa ndani ya msikiti wake alimuomba Bi ‘Aisha akiwa ndani ya chumba chake hali ya kuwa yuko katika siku zake ampe kitu, Bi ‘Aisha alimwambia Mtume Swalla LLahu ‘Alayhi Wasallama kuwa yuko katika siku zake; ndipo Mtume akamwabia hedhi yako haiko mkononi mwako. Jibu ni kuwa hakuna sharti la tohara ktk kukata viungo hivi ila kilichoelezwa na sheria ni kuwa vinapoondolewa vihifadhiwe kwa kufukiwa na si kutupwa ovyo na hii ni kwa kuwa mwili wa mwanadamu ni mtukufu na hivyo viungo vyake pia ni vitukufu na hivyo vyatakikana vihifadhiwe kwa kuwekwa sehemu maalumu na sehemu bora zaidi ikawa ni kuvifukia chini ya ardhi kuliko kuvitupa ovyo au kuvichoma. Pia hili ni jambo miongoni mwa majambo yanayoonyesha uislamu na uhifadhi wa mazingira.

Ewe dada yangu katika Uislamu Mwenyezi Mungu na Mtume wake wameweka mipaka tusiikaribie na miongoni mwa mipaka ya Allah ni wanawake kutokujipulizia perfume au udi au manukato mbalimbali yenye kuweza kuwafanya wanuswe na wanaume wasio Maharimu zao. Hili ni haramu na Sheria imelikataza kwa makemeo mazito sana! Hii haina maana kuwa mwanamke awe ananuka kikwapa.

KATAZO LA MWANAMKE KUTOKA NJE HUKU AKIWA AMEJITIA MANUKATO AU UDI.
Moja katika madai ya wanawake ni kuwa mtu si vizuri kusikiwa harufu mbaya [majasho]; juu ya kuwa kuna waume ambao hawasikii harufu nzuri za wake zao isipokuwa pale wanapotoka kwenda katika maharusi; katika kulidhibiti hilo huwa wanapotoka kwa kutaka kutimiza mahitajio yao, kwenda shughulini au shughuli zao za kawaida hujitia manukato yenye kuhanikiza, udi, mafuta mazuri, mafuta ya nywele yenye kunukia au mafuta ya kujipaka mwilini yenye kunukia au hata wanapokoga hutumia sabuni zenye kunukia ili wawe na harufu wanapotoka; desturi hii inawapeleka wengine kushikamana nayo hata wanaposaidiwa kupelekwa pahala kwa gari iwe ya kulipa au ya rafiki wa mume [akiwa na huyo mume mwenyewe ndani ya gari] au hata kwenda Misikitini hujimwagia manukato na kusikiwa na kila mtu awe mpita njia, dereva, na kadhalika.
Kwa anayeelewa basi huu ni msiba, na msiba huwa mkubwa zaidi kwa asiyeelewa; kwani jamii yaonyesha kuwa si kuwa iko mbali tu na mafundisho aliyokuja nayo Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), bali jamii imeyatupa mbali na kuyadharau mafundisho na kila lenye kuambatana na mafundisho hayo.
Kutoka kwa bibi Zaynab ath-Thaqafiyyah (Radhiya Allaahu 'anhaa) kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: "Atakapo shuhudia mwanamke mmoja wenu Swalah ya 'Ishaa [na katika riwaayah: Msikitini] basi asiguse manukato usiku huo” [Imepokelewa na Muslim, kitabu cha Swalah, mlango wa kutoka wanawake kwenda Misikitini ikiwa haitosababisha fitnah na hali yeye..., Hadiyth namba 678 na namba 679].
Na kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema kwamba amesema Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Mwanamke yeyote yule ataejifukiza udi [harufu nzuri] basi asishudie pamoja nasi Swalah ya ‘Ishaa ya mwisho” [Imepokelewa na Muslim, kitabu cha Swalah, mlango wa kutoka wanawake kwenda Misikitini ikiwa..., Hadiyth namba 680.]
Na kutoka kwa Abu Muusa Al-Ash-‘ariy (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema kwamba amesema Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ”Mwanamke yeyote yule ataejitia manukato akapita mbele ya watu ili waipate harufu yake basi huyo ni mzinifu [atakuwa amezini]” [Imepokelewa na Ahmad katika musnad wake, kitabu Musnad wa watu kumi waliobashiriwa pepo, hadiyth ya Abi Musa Al-Ash-‘ariy (Radhiya Allaahu 'anhu), Hadiyth namba 19272 na 19305; na at-Tirmidhiy, katika Kitabu cha Adabu, mlango wa yaliyokuja katika yenye kuchukiza kutoka kwa mwanamke ..., Hadiyth namba 2730].
Hadiyth hizi zote dada yangu katika iymaan zinathibitisha uharamu wa kutoka nyumbani kwako hali ya kuwa unanukia, kwani manukato au harufu yake haraka huwafanya wanaume wavutiwe na kupata matamanio ya kutaka kumkaribia aliyejipaka hayo manukato.
Katika kusherehesha neno [huyo ni mzinifu] Wanazuoni wanasema kuwa “Amezini kwa kuwa amesababisha kuzindua matamanio ya wanaume kwa hiyo harufu wanayoipata inayotokana na manukato [au udi] aliojitia; jambo linawapelekea kutaka kuelewa nani huyo mwenye kunukia na hilo huwapelekea kumkodolea macho; na mwenye kumtazama huwa amezini [zinaa ya macho], kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ameandikiwa kila mwanaadamu sehemu yake katika zinaa; hakuna njia ya kuiepuka; macho mawili zinaa yake ni kutazama, masikio mawili zinaa yake ni kusikiliza, na ulimi zinaa yake ni kusema, na mkono zinaa yake ni kuunyoosha, na mguu zinaa yake ni hatua zake, na moyo hupata matamanio, na tupu husadikisha au kukadhibisha” [Imepokelewa Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Tafsiyr Qur-aan, Suurat Qul A’uwdhu birabbil Falaq, Hadiyth namba 6152; na Muslim, katika Kitabu cha Qadar, mlango wa imekadiriwa juu ya kila mwanaadam sehemu yake katika zinaa, Hadiyth namba 4808 na namba 4809].
Ni jambo linaloeleweka kuwa kumtazama mwanamke ni katika vitangulizi vya zinaa ya sehemu za siri za wanaume, hivyo ni wajibu kwa kila dada mwenye kuamini Allaah na Siku ya Qiyaamah kutotoka nyumbani kwake isipokuwa kwa haja [dharura] yenye kukubalika na Shariy’ah, na hapo atapohitaji kutoka, basi ahakikishe kuwa anajipamba kwa adabu za kishariy’ah ambazo miongoni mwake ni kuwa amejifunika na kujisitiri vizuri kwa hijabu ya kishariy’ah; na wakati wowote ule ataporudi nyumbani kwake yuko huru kujitia manukato atakavyo, kwa sharti kuwa hawatoipata harufu ya manukato yake wanaume wengine wasio kuwa maharimu zake.
MWANAMKE KUDHIHIRISHA MAPAMBO KWA WANAUME
Allaah Aliyetukuka Anasema kuwaambia wanawake: {Na kaeni majumbani kwenu, wala msijishauwe kwa majishauwo ya kijaahiliyyah...…} [Al-Ahzaab 33: 33].
Amesema Mujaahid: “Walikuwa wanawake wanapotoka nje ya nyumba zao hujipitisha mbele za wanaume, na huko ndiko kujishauwa kwa majishauwo ya kijaahiliyyah.”
Amesema Qataadah: “Walikuwa wanawake wanapotoka nje ya nyumba zao, hutembea ovyo pasina hayaa na huku wakijitikisa tikisa, na ndio Allaah Aliyetukuka Akawakataza.”
Amesema Muqaatil bin Hayyaan: Tabarruj ni pale mwanamke anapokuwa ameweka Khimaar [shungi] kwenye kichwa chake lakini akawa hakuifunga itakiwavyo, hivyo mkufu [kidani], vipuli [herini], shingo yake na vyote hivyo vikawa vinaonekana”.
Wanawake wanakatazwa kujishauwa na kujitikisatikisa wakati wakiwa wako nje ya nyumba zao; na huwa ubaya zaidi pale wanapokuwa wamejipamba kwani kutawapelekea wanaume wawatazame na kuyaona mapambo yao; wanawake hawa huwa na mitindo ya kimaajabu ya kupiga viatu vyao chini na kadhalika.
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Aina mbili za watu ni miongoni mwa watu wa Motoni sijawahi kuziona: Watu ambao wana fimbo [mijeledi] kama mikia ya ng'ombe dume ambazo wanawapigia watu, na wanawake ambao wamevaa lakini wako uchi; wanawashawishi wanaume wawatongoze, na wanaelekea kwao [kwa kuwa warahisi]; vichwa vya wanawake hao kama nundu za ngamia zinazoyumba; hawatoingia Peponi na wala hawatoipata [hawatosikia] harufu yake, na harufu yake inaweza kusikiwa kutoka masafa kadhaa na kadhaa [Imepokelewa na Muslim, kitabu cha Jannah na sifa za na’iyma zake na watu wake, mlango wa Moto watauingia majabari na Pepo wataiingia madhaifu, Hadiyth namba 5103; na katika Kitabu cha Mavazi na mapambo, mlango wa wanawake Al-Kaasiyaat Al’Ariyaat Al Maailaati.., Hadiyth namba 3978].
Angalia dada yangu katika Iymaan makemeo makali hayo na mazito na adhabu inayomsubiri mwenye kujifakharisha kwa uzuri wake na kudhihirisha mapambo yake kwa wanaume wasio kuwa maharimu zake; huenda kwa mwanamke kudhihirisha mapambo yake kwa wanaume hapa duniani ikawa furaha, fakhari, pato zuri [kama wenye kushiriki katika mashindano ya mwanamke mzuri] tija na umaarufu; lakini itakuwa hasara na majuto Siku ya Qiyaamah, kwani itakuwa ni sababu tosha kwa yeye kujiharamishia Jannah na kutumbukizwa Motoni.
Ewe mwenye kuamini Allaah na Siku ya Qiyaamah! Jihadhari na kudhihirisha mapambo yako kwa wanaume wasiokuwa maharimu zako; jihadhari sana na kutojisitiri vizuri kwa hijabu ya kishariy’ah utokapo nje ya nyumba yako, au hata ndani ya nyumba yako wakiwepo wasiokuwa maharimu zako; jihadhari na kujitia manukato, udi na mfano wa hivyo wakati unapotoka nje ya nyumba yako; jihadhari na kupatikana harufu ya manukato yako na wanaume wasiokuwa maharimu zako; yote hayo dada yangu katika iymaan ubaya wake ni wenye kuchukiza kwa Mola wako na ni katika yenye kukupelekea kuwa miongoni mwa wenye kuwajibikiwa adhabu Siku ya Qiyaamah.

MAVAZI YA MWANAMKE HARUSINI NA ANAPOKUWA NA WANAWAKE WENZAKE.

 

Wanawake wengi wa Kiislamu huvaa nguo za wazi kabisa wanapohudhuria harusi, kama vile kanzu fupi zinazoonyesha miguu au mikono yao yote kuwa wazi au kuvaa bega moja na moja liko wazi, baadhi ya kifua kuwa wazi, au nguo za kubana (tight) hadi mwili wote au viungo vyake kuonekana, au mgongo kuwa wazi n.k. Hali huwa mbaya zaidi katika makumbi ya sherehe ambapo wanawake wanaokuja haki ya kuwa wamevaa nguo fupi au mtu anaona vilivyomo ndani ya nguo, au mavazi na miundo ya kukatwa ambayo inaonyesha vya ndani kabisa, au wanavaa nguo za kuonyesha mwili na maungo ya ndani kabisa, au vazi linaloonyesha sehemu ya kifua au sehemu ya nyuma wazi. Utadhani wanawake hao wanatoka nje na wanaonekana au ni wachezaji sinema katika nchi za kikafiri!

 

Je ikiwa wanawake wakiwa mbele ya wanawake wenzao tu ni ipi mipaka ya mavazi baina yao? Je ni kweli kwamba 'awrah (uchi) wa wanawake mbele ya wanawake wengine ni kutoka kitovuni na magotini? Je hili ni sahihi?


Mwanamke (mwili wake wote) ni 'awrah mbele ya wanaume ambao si Mahrim zake (anayeweza kumuoa), na haijuzu kwake kuonekana mbele ya wanaume hata kama atakuwa ni mwenye kujisitiri, kwa kuhofia fitnah kwa kumuangalia na kuona jinsi alivyo na jinsi anavyotembea. Ama kuhusiana na kuwa 'awrah ya mwanamke mbele ya wanawake wenziwe ni kutoka kitovu hadi magoti, hii inatumika tu wakati atakapokuwa kwenye nyumba yake na dada zake na wanawake ambao anaishi nao. Pamoja na haya Kanuni za msingi bado zinasisitiza mwanamke asitiri mwili wake wote ili achukuliwe kama kiigizo bora. Vile vile, anapaswa kusitiri uzuri wake mbele ya mahrim wake na wanawake wageni ili baadhi ya mahrim wake wavutiwe (waathirike) nae kitabia na adabu, au ili baadhi ya wanawake wasije kwenda kumuelezea yeye wasifu wake kwa wengine (wanaume). Imeripotiwa katika Hadiyth kuwa Mtume (Swala Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema: "Haitakiwi mwanamke kumuelezea mwanamke mwengine kwa mume wake, hivyo ni kama (mumewe) anamuona yeye" Kinachomaanishwa hapa ni uzuri wake, kama vile kifua chake, mabega yake, tumbo lake, nyuma, mikono yake, shingo yake n.k, vyote hivi vinakuwa wazi, kila mtu anaona kwamba, ni jambo lisiloweza kuepukwa, mtu kupatwa na hisia zake.

Inaweza kuwa jambo la kawaida kabisa kwa wanawake kuelezea wanamume na wanawake waliyoyaona kwa wanawake hao kwa familia zao au hata zaidi ya hapo. Hivyo mwanamke anaweza kuyataja hayo mbele ya watu ambao si Mahrim wake, kwa namna ambayo inaweza kuwafanya wao kuvutiwa kwake [huyo mwanamke], au ambayo inaweza kusababisha watu wabaya kutafuta njia kuanzisha uhusiano naye. Kwa sababu hii, wanawake wanatakiwa kufunika 'awrah [sehemu zisizotakiwa kuonekana katika miili] yao - kama vile vifua vyao, migongo, mikono, ndama, n.k; vile vile hata mbele ya mahrim wake na wanawake wengine. Kujisitiri huku kunakuwa muhimu zaidi katika sehemu za makundi, maeneo ya sherehe, hospitali, na shuleni, hata kama kutakuwepo wanawake tu, kwa sababu baadhi ya wanaume ambao si Mahrim na hata vijana wanaweza kuwaona au kuwachukua picha hali ya kuwa hawana stara zao kamili, na hiyo itakuwa ni sababu ya fitnah kwa wale wanaowaona. Onyo kali imetolewa kwa wale [wanawake] ambao wanajionyesha na wavaao nguo za kuonyesha au za kubana, wakati Mtume (Swala Allaahu 'alayhi wa sallam) aliposema: Aina mbili za watu wa motoni siwaoni... Wanawake ambao wamevaa lakini wako uchi, wanawashawishi wanaume wawatongoze, na wanaelekea kwao (kwa kuwa warahisi). Vichwa vyao kama nundu za ngamia zinazoyumba (aina ya msuko wa nywele wanaosuka wanawake). Hawataingia Peponi wala hawatasikia harufu yake ingawa harufu yake inaweza kunuswa kutoka masafa kadhaa na kadhaa” [Muslim].

Kinachomaanishwa katika hadithi hii ni kwamba wamevaa nguo za kuonyesha au nguo za kubana ambazo zinaonyesha maumbile yao, au kunapokuwepo fursa ya ajira kwenye kampuni ambayo [mavazi yao] huonyesha vifua vyao, matiti yao na sehemu zingine zisizofaa kabisa kuonekana.

Ama kuhusiana na mwanamke kuruhusiwa kudhihirisha nywele zake mbele ya wanawake wengine na mahrim wake, kamati ya kudumu (al-Lajnah al-Daa'imah) ya Utafiti wa Elimu na mas-ala ya Fatwa wana maelezo yafuatayo juu ya suala hili, ambayo inasomeka kama ifuatavyo: “Waumini wanawake mwanzo wa Uislamu walikuwa safi sana, wenye hayaa na wenye aibu, jambo ambalo ilikuwa ni baraka ya imani kutoka kwa Allaah na Mtume Wake, na walikuwa wakifuata Qur-aan na Sunnah. Wanawake katika kipindi hicho walikuwa na ada ya kuvaa nguo za kujisitiri, na haikujulikana kwamba walikuwa wakijifunua wanapokutana na mmoja au wanapokutana na mahrim zao. Wanawake wa ummah huu wanatakiwa wafuate tabia hii nzuri kizazi baada ya kizazi mpaka hivi karibuni. Lakini wakati uharibifu na fitnah zilipoingia kwa wanawake, njia ya mavazi yao na wanavyojiweka kwa sababu nyingi (inasikitisha sana), jambo ambalo hatuna nafasi ya kulijadili hapa. Kwa sababu ya idadi kubwa ya maswali ambayo yametumwa kwenye Kamati ya Kudumu ya Utafiti wa Elimu na Fatwa kuhusu wanawake kuangalia wanawake wenzao, na nini anachopaswa mwanamke kuvaa, Kamati inawaambia wanawake wote wa Kiislamu kwamba wanawake ni wajibu kwao kuwa na tabia ya kuwa na hayaa, jambo ambalo Mtume (Swala Allaahu 'alayhi wa sallam) alielezea kuwa ni sehemu ya imani na moja ya matawi ya imani. Suala la hayaa ambalo ni amri iliyotolewa na Uislamu na kwa desturi ni kuwa wanawake wanapaswa wajisitiri, kuwa na hayaa, tabia na maadili ambayo yatawaweka mbali na kuanguka katika fitnah (majaribio) na hali ya utata. Qur-aan inaonyesha wazi kuwa mwanamke hapaswi kuonyesha wanawake wengine chochote zaidi ya wanawake ambao ni Mahrim wake, hali ambayo ni ya kawaida yeye kujifunua katika nyumba yake ni wakati wa kufanya kazi za nyumbani, kama jinsi Allaah Anavyosema: “…wala wasionyeshe uzuri wao isipo kuwa unaodhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao,” [An-Nuur 24:31]. Ikiwa haya ndiyo maandiko ya Qur-aan na ndiyo latambulikana katika Sunnah, basi hili ndilo ambalo wake wa Mtume (Swala Allaahu 'alayhi wa sallam) na wanawake wa Maswahaba walivyokuwa wakifanya, na wanawake wa Ummah ambao waliwafuata kwa wema mpaka siku ya leo.

Jambo la kawaida la wanawake kujifunua ni wakati wao wako nyumbani na wakati wanafanya kazi za nyumbani, hali ambayo ni vigumu kujizuia, kama vile kujifunua kichwa, mikono, shingo na miguu. Tukienda upande wa kuvuka mipaka katika kujifunua, hakuna dalili katika Qur-aan na Sunnah kwamba inajuzu. Hii pia ni njia inayoongoza kwa mwanamke kumjaribu au kujaribiwa kwa wanawake wengine, ambayo hufanyika kati yao. Pia inakuwa ni mfano mbaya kwa wanawake wengine, kama vile kuwaiga wanawake wa Kikafiri, makahaba na wanawake waovu jinsi wanavyovaa. Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swala Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema: “Yeyote atakayeiga (jifananisha) na watu basi atakuwa miongoni mwao.”  (Imepokelewa na Imaam Ahmad na Abu Daawuud). Katika Swahiyh Muslim (2077). Imesimuliwa kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amr kuwa Mtume (Swala Allaahu 'alayhi wa sallam) alimuona amevaa nguo mbili za hariri, akasema: “Haya ni katika mavazi ya makafiri, usiyavae.” Pia imepokelewa katika Swahiyh Muslim (2128) Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allahu 'anhu): Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Aina mbili za watu wa motoni siwaoni; Watu ambao wana fimbo (mijeledi) kama mkia wa ng'ombe dume ambazo wanawapigia watu, na wanawake ambao wamevaa lakini wako uchi, wanawashawishi wanaume wawatongoze, na wanaelekea kwao (kwa kuwa warahisi). Vichwa vyao kama nundu za ngamia zinazoyumba (kwa mtindo wa nywele wanaosuka). Hawataingia Peponi wala hawatasikia harufu yake ingawa harufu yake inaweza kunuswa kutoka masafa kadhaa na kadhaa.” Maana ya kauli hii “wamevaa lakini wako uchi” ni kwamba mwanamke amevaa nguo ambayo haijamsitiri, kwa hiyo amevaa, lakini kwa staili ambayo bado yuko uchi, kama vile wakati anavaa nguo nyembamba ambayo inaonyesha rangi ya ngozi yake, au vazi ambayo inaonyesha hali ya mwili wake, au vazi fupi ambalo halisitiri sehemu za viungo vyake.

Kwa hiyo, jambo ambalo wanawake wa Kiislamu wanapaswa kufanya ni kushikamana na uongofu waliokuwa wakifuata mama wa Waumini (wake wa Mtume) na wanawake wa Maswahaba (Radhi za Allaah ziwashukie), na wanawake wa ummah huu ambao wanawafuata hao kwa wema, na wajitahidi kujisitiri na kuwa na hayaa. Hili litawafanya kuwa mbali kuwasababishia fitnah na litawalinda na mambo yanayosababisha uchochezi wa tamaa na kuanguka katika zinaa. Waislamu wanawake wanapaswa kujihadhari kuanguka katika mambo ambayo Allaah na Mtume wamekataza, kama kuwaiga wanawake wa kikafiri na makahaba.  Kila Muislamu pia (mwanaume) anapaswa kumuogopa Allaah kuhusiana na wanawake ambao wako chini ya ulinzi wake, na kutowaacha wakavaa mavazi ambayo Allaah na Mtume Wake wameharamisha, kama vile nguo za kuvutia, au mavazi ambayo ni ya kudhihirisha maumbile na uchi, au yale ya majaribio (fitnah) ya kuwashawishi watu. Anapaswa kukumbuka (mwanaume) kuwa yeye ni mchungaji na ataulizwa kwa alichokichunga siku ya Qiyaamah.

Kwa mantiki ya haya haifai mwanamke kumuonyesha uchi mwanamke mwenzake. Kwa hiyo kisheria haifai mwanamke kumfunulia mwanamke mwenzake kitovu chake, mapaja au matiti yake kwa madai eti anapakwa hina na mfano wake. Jambo hili limekatazwa Kisheria kwani anayeruhusiwa kuona sehemu hizo ni mume peke yake. Kwa maelezo zaidi juu ya haya tazama Fataawa al-Lajnah al-Daa'imah, 17/290 na pia Fataawa al-Lajnah al-Daa'imah (17/297): “Nini ambacho mwanamke anaruhusiwa kudhihirisha mbele ya watoto wake ni yale mambo ambayo kidesturi huwa wazi, kama vile uso, mikono, miguu, na kadhalika. Ama kuhusiana na kipi kiasi kinachochukuliwa kuwa ni 'awrah kwa mwanamke awapo na wajomba zake kwa upande wa mama, wajomba zake upande wa baba na ndugu zake, nyumbani? Jibu ni kuwa anaruhusiwa kuonyesha kwa Mahrim wake: uso, kichwa, shingo, mikono, miguu, chini ya muundi, na anapaswa kusitiri kila kitu mbali na hivyo tulivyotaja”. Tazama Shaykh Muhammad bin Swaalih al-‘Uthaymiyn Hijaab Mar-ah wa ziynatuha, ukurasa wa 43.

Nikumbushe tu jambo hapa kuwa haifai wanawake kuoga pamoja. Hili ni jambo ambalo limekatazwa Kisheria na linaweza kuwa sababu ya wanawake kusagana; moja kati ya madhambi makubwa ambayo adhabu yake inaweza kuwa adhabu ya kifo kwa msagaji na msagwaji!

MWANAMKE KUVAA MIKUFU MIGUUNI
Hakuna ubaya kwa mwanamke kuvaa mkufu miguuni na hata pete katika vidole vya miguu ikiwa ni kwa ajili ya kujipamba kwa mumewe. Na wala asidhihirishe mapambo hayo nje kwa wasiomhusu, yaani wasio maharimu zake wasiyaone katu na ikiwa watayaona mwanamke huyo anapata dhambi lukuki. Dalili ya haya tunaipata katika aya ya hijaab inayomalizia kukataza wanawake wanaovaa mikufu miguuni mwao wasitembee kwa kupiga miguu yao hadi ijulikane kuwa wamevaa mapambo hayo miguuni mwao: {Wala wasipige chini miguu yao ili yajulikane mapambo waliyoyaficha} [An-Nuur: 31]
Hii ni wazi pia kuwa hijaab ya sheria inampasa mwanamke ajifunike hadi miguuni mwake. Tunaona dada zetu wengi wanajifunika tokea juu lakini miguu yao iko wazi hata katika Swalah utawaona wanaswali na miguu/vidole vya miguu vinaonekana. Swalah zao hawa zinakuwa hazikukamilika kwani mwanamke anatakiwa ajifunike kote isipokuwa uso tu na viganja vya mikono.
MASHARTI YA HIJAAB

Ama kuhusu masharti kwa vazi la kike kuitwa la Kiislamu au Hijaab ni kama yafuatayo:

1.   VAZI LA MWANAMKE WA KIISLAMU NI LAZIMA LISITIRI MWILI MZIMA: Wanachuoni wametofautiana kuhusu viganja vya mkono na uso kwa kauli mbili – wapo wanaosema ni lazima vifunikwe na wanaokubali kuwa vinafaa viachwe. Wengine wameunganisha kauli hizo kwa kusema hadi ya chini ni kuacha vitanga vya mkono na uso kuwa wazi lakini vikifunikwa ni bora zaidi. Kuhusu kusitiri tayari tumenukuu aayah mbili za Suratun Nuur Aayah ya 31 na Suratul Ahzaab Aayah ya 59.

2.   VAZI LENYEWE LISIWE NI PAMBO: Hii ni kwa kauli ya Aliyetukuka: “Wala wasionyeshe uzuri wao isipokuwa unaodhihirika” (an-Nuur 24: 31). Na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Watu aina tatu hata usiwaulize: … Na mwanamke ambaye mumewe hayupo lakini amemtosheleza na mahitaji yake yote ya kidunia, naye akafanya Tabarruj (Ahmad na al-Haakim). Tabarruj ina maana mwanamke kuonyesha pambo lake na uzuri wake ambao unatakiwa usitiriwe, ambavyo vinamfanya mwanamme awe na matamanio. Na kusudio la amri ya kuvaa Jilbaab ni kusitiri pambo la mwanamke, hivyo haingii akilini iwe Jilbaab lenyewe liwe ni pambo.

3.   VAZI LIWE ZITO, KISIONEKANE KILICHO NDANI YAKE: Hii ni kwa kauli yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Watu aina mbili wa Ummah ni wa Motoni nami sijawaona… na wanawake waliovaa nguo lakini wapo uchi. Hao hawatoingia Peponi wala hawatopata harufu yake japokuwa harufu yake inafika masafa kadhaa na kadhaa” (Muslim). Lengo ni kwa wale wanawake wanaovaa nguo hafifu ambayo inatoa sifa kamili na wala haisitiri. Hao kwa jina wamevaa lakini kwa uhakika wako uchi.

4.   VAZI LIWE PANA, SIO LA KUBANA: Kwani vazi likimbana mwanamke litamtoa umbile lake lote hivyo kumfanya kama kwamba hajajisitiri. Hii ni kwa mujibu wa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumwambia Usaamah bin Zayd (Radhiya Allaahu ‘anhuma): “Muamuru mkeo ajaalie Ghulaalah (shuka inayovaliwa chini ya nguo), kwani nakhofia isije ikasifu ukubwa wa mifupa yake” (Ahmad na Abu Daawuud).

5.   VAZI LISITIWE MANUKATO: Hii ni kutokana na kauli ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mwanamke yeyote anayejitia manukato, akawapita mbele ya watu ili wapate harufu yake, basi yeye ni mzinifu” (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy).

6.    VAZI LISIFANANE NA VAZI LA KIUME: Huku ni kwa kule kulaaniwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wanaume wanaoshabihiana na wanawake na wanawake wenye kujifananisha na wanaume (al-Bukhaariy, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah). Na pia amesema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) “amelaaniwa mwanamme mwenye kuvaa nguo za kike, na mwanamke mwenye kuvaa nguo za kiume” (Ahmad na Abu Daawuud).

7.   VAZI LISIFANANE NA VAZI LA KIKAFIRI: Shari’ah imekariri kutojuzu kwa Waislamu wanaume kwa wanawake kujifananisha na makafiri sawa katika ‘Ibaadah, au sherehe, au katika mavazi yao na kadhalika. Ama kuhusiana na kivazi, ni ile Hadiyth ya ‘Abdullaah bin ‘Amru (Radhiya Allaahu ‘anhuma) aliyesema: “Alimuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa amevaa nguo mbili za njano, akamwambia: “Hakika hizi nguo ni za makafiri kwa hivyo usivae” (Ahmad, Muslim na an-Nasaa’iy).

8.   VAZI LISIWE NI LA KUJIONYESHA: Hii ni kwa kauli yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mwenye kuvaa nguo ya umaarufu na kujionyesha hapa duniani, Allaah Atamvisha nguo ya udhalili Siku ya Qiyaamah, kisha Atamuingiza Motoni” (Abu Daawuud na Ibn Maajah). Haya ndio masharti ambayo yanafaa yawepo katika vazi la mwanamke ili lijulikane kuwa ni la Kiislamu. Ikikosekana sharti hata moja basi litakuwa vazi lenyewe si la Kiislamu. Kwa ajili hiyo, ma ‘Abaaya mengi hayatimizi masharti haya wala yale mabaibui ya fasheni. Nasaha kwa dada zetu waepukane na hayo.


KUWAJIBIKA KWA HIJAAB


Yuko mtu mmoja aliwahi kusema: Pombe na mwanamke vinaweza kuwaangamiza Waislamu kuliko mizinga mia moja wazamisheni katika kupenda vitu hivyo. Imekuwa dhahiri siku hizi maadui wa Waislamu wanapotaka kuangamiza kuwangamiza Waislamu, kitu cha kwanza wanachoathiri ni mwanamke! Kwasababu mwanamke akipoteza stara yake, ni rahisi kwa vijana pia kupotea, hivyo basi ni rahisi kwa jamii nzima kupoteza stara yao. Kwahivyo tukisema stara kwa mwanamume ni wajibu, basi kwa mwanamke pia ni wajibu, na ni mujibu. Kwa ajili ya tabia ya mwanamke ya kuwa na haya, ni rahisi kwake kuwa karibu na stara. Na kitu muhimu kabisa kwa mwanamke ni kujihifadhi na kujifunika mwili wake. Kitu kikubwa anachomiliki mwanamke, ni Hijaab yake. Kwa kaka na dada wanaosoma haya, someni na muwafahamishe dada zenu na jamaa zenu kwani tunaambiwa tuokoe nafsi zetu na za jamaa zetu na moto. Dada yangu katika Uislamu, ikiwa unasoma haya, ilihali wewe ni muhajjaba (mwenye kuvaa Hijaab), basi eneza risala hii kwa dada zako wa kiislamu, na ikiwa wewe sio muhajjaba, basi jaribu upate faida kutokana na haya.
Kama nilivyosema kitu kilichotukuka kabisa ambacho mwanamke anamiliki, ni stara. Na kitu cha thamani katika stara ni Hijaab. Nikikuuliza kitu gani cha thamani unachomiliki, itakuwa ni nini? Ukiwa na kitu cha thamani, utakitunza na kukihifadhi? Utakificha au la? Ukiwa na lulu au johari, je, utaihifadhi mahali pazuri au la? Kila thamani yake ikizidi, basi utazidi kutaka kuihifadhi. Hivyo basi, utaificha watu wasiione. Au utaionyesha na kuiweka wazi mbele ya kila mtu aione na achukue atakacho kutokana nayo?
Hakika utaihifadhi! Vile vile, mwanamke ni kiumbe mwenye thamani kubwa kwa hivyo inampasa ajihifadhi.
Dada, je, unajua kama lulu inahifadhiwa na ganda lake? Kweli au si kweli? Kwa hivyo huwezi kuwa mwenye kuhifadhika bila ya Hijaab kwani Hijaab inakuhifadhi na fitna nyingi.
Mwanamke ni lazima ajistiri kwa kuvaa Hijaab kwa sababu ni rahisi sana mwanamume kumtongoza yeye kwa uzuri wake.
Kabla ya Uislamu kutujia, mataifa mengi yaliamini kuwa uzuri wenye thamani unapatikana katika mwili wa mwanamke peke yake. Uislamu ulipokuja ulibadili fikra hizo kwa kufundisha watu kuwa uzuri wa mwanamke sio wa mwili peke yake, bali ni wa tabia, fikra na mengineyo mengi.
Haijaandikwa kabisa sheria ya kuwa mwanamke lazima ajioneshe uzuri wake. Hakuna apasae kuuona wala kuufaidi uzuri wake isipokuwa mumewe. Watu aina gani wanampa mwanamke heshima anayostahiki? Watu ambao wanamfanya mwanamke ajioneshe uzuri wake, au wenye kumfundisha ajistiri uzuri wake ila kwa wale wanaostahiki kumuona uzuri wake? Wengine wanadai kuwa Hijaab sio wajibu. Tuangalie Qur-aan inasema nini kuhusu Hijaab.
{Ee Mtume waambie wake zako, na binti zako, na wanawake  wa Kiislamu wajiteremshe uzuri nguo zao.  Kufanya hivyo kutapeleka upesi wajulikane (kuwa ni watu wa heshima) wasiudhiwe. Na Allaah ni Mwingi wa kusamehe (na) Mwingi wa kurehemu } [Al-Ahzaab 33: 59].

Tuzingatie kuwa Allaah anapozungumzia kuhusu Hijaab kuwa wajibu, Amejumuisha wanawake wenye kuamini pia, sio wake za Mtume  peke yake, kwa hivyo ni wazi kuwa aya hii haikuteremshwa kwa jamii ya Mtume pekee, imeteremshwa kwa ajili ya kuhifadhi wanawake wote. Kwa hivyo wanawake wote wenye kuamini ni lazima wavae Hijaab ili waheshimiwe na wajulikane kuwa ni wenye haya. Hakuna atakaemdhuru kwa ajili ya heshima aliyojiwekea juu ya mavazi yake.
Hijaab ni lazima! Allaah Anasema: {Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipo kuwa unao dhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao, au iliyo wamiliki mikono yao ya kuume, au wafwasi wanaume wasio na matamanio, au watoto ambao hawajajua mambo yaliyo khusu uke. Wala wasipige chini miguu yao ili yajuulikane mapambo waliyo yaficha. Na tubuni nyote kwa Allaah, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa} [An-Nuwr 24: 31].
Wataalamu wengi wanasema kuwa ni lazima wanawake wajifunike  mwili wote isipokuwa viganja vya mkono na uso. Allaah Aliposema wanawake wavae Khimaar, Hakumaanisha kuwa wavae leso kubwa tu, bali ni kuwa mwanamke akivaa hiyo Khimaar, itamfunika mapambo yake muhimu, nayo ni masikio, shingo na kifua. Kwa hivyo, mwanamke akivaa kitambaa kidogo ambacho hakimsitiri mapambo yake hayo tuloyataja, basi hiyo sio Hijaab.

Baada ya kuona katika Qur-aan kuwa Hijaab ni wajibu, inampasa mume kumhimiza mkewe na kumshawishi avae Hijaab ili aheshimiwe na athaminiwe kuwa ni mchaji Allaah. Katika aya nyengine Allaah  anawahutubia wanawake wa Kiislamu wasioneshe mapambo yao kama walivyokuwa wakifanya wanawake wakati wa jahilia (kabla Uislamu). Wanawake wa jahilia walikuwa wakivaa nguo ndefu lakini mapambo yao yote yalikuwa yakionekana, kama vile shingo, masikio, nywele na kadhalika.
Aayah ya Hijaab ilipoteremka tu, wanawake wote walitoka huku wamevaa Hijaab. Wanaume waliposikia aya hiyo waliwaeleza wanawake maana yake, basi wanawake walikuwa tayari Kufuata shari'ah ya Allaah kama alivyoieleza katika Qur-aan. Madhali walikuwa hawana uwezo wa kununua nguo mpya, walinyanyua nguo zao kwa sehemu mbili ili watumie kama Hijaab. Hiyo ni kinyume na vile wanawake wakisasa walivyo. Wao hutoa visingizio kwa kutovaa Hijaab inayotakikana. Mtume alisema: “Kikundi cha wanawake hawatoingia peponi. Hao ni miongoni mwa wale wanaovaa nguo za kubana, za kuonyesha mwili na hawafuati amri ya Allaah ya kuvaa Hijaab. Hawataingia tu peponi bali hata hawatasikia harufu ya pepo ambayo harufu yake husikilizana masafa ya mwendo wa miaka 500.” [Muslim].    
Kutilia mkazo umuhimu wa kujifunika, ilimbidi Mtume alipige vita kabila moja la Kiyahudi ambalo lilimchezea shere mwanamke wa Kiislamu sokoni. Walimfanyia hila huyo mwanamke kwa kuifunga nguo yake ili akitembea aanguke na nguo yake ipasuke kisha awe uchi. Basi mwanamume mmoja aliyeshuhudia hayo, alipigana na kumuuwa yule Yahudi aliyefanya mambo hayo. Mtume aliamrisha jeshi lake liwafukuze kabila hilo la Kiyahudi nje ya Madinah.
 SABABU ZA WANAWAKE KUTOVAA HIJAAB
1.   SIJASADIKIKA NA HIJAAB
Sasa nitakuuliza wewe ni nani? Utajibu wewe ni Muislamu. Uislamu unaamanisha nini? Uislamu ni kumtii Allaah kabisa kwa mambo yote aliyotuamrisha. Na kuvaa Hijaab ni mojawapo ya maamrisho ya Allaah wanamke ambae hataki kuvaa Hijaab basi hajamtii Allaah.
2.   MADAI YA KUWA NIA NDIYO KITU MUHIMU
Mwanamke ambae anadai kuwa kitu muhimu ni nia yake, na kuwa dhamira yake sio mbaya na kuwa yeye ni mtu mzuri, na kuwa Hijaab ni ya moyo. Mwanamke huyo huyo anadai kuwa anaswali swala tano, sunna na swala za usiku na anatoa sadaka. Kweli anafanya yote hayo, lakini kisha anasema ibada hizo zinatosha. Subhana Allaah!   Kasema Allaah: {Je! Mnaamini baadhi ya Kitabu na mnakataa baadhi yake? Basi hana malipo mwenye kutenda hayo miongoni mwenu ila hizaya katika maisha ya duniani, na Siku ya Qiyaamah watapelekwa kwenye adhabu kali kabisa. Na Allaah si mwenye kughafilika na yale mnayo yatenda}.  [Al-Baqarah 2: 85].
Kwa hivyo tufanye hisabu, unasema unafanya mengi mema, kuwa nia yako ni nzuri na moyo wako ni msafi. Sawa, lakini kila siku unapotoka, wanaume wangapi wanakuangalia nywele zako, na uzuri wako wote, je unakusanya madhambi tele au la? Hakika unakusanya madhambi kwasababu hukufuata amri ya Allaah. Na huyu mwanamke atashindana kuwa sio makosa yake wanaume wakimuangalia kwasababu nia yake sio mbaya, bali atasema kuwa wanaume ndio watakao pata madhambi. La hasha! Wewe ndio chanzo cha hao wanaume kukuangalia kwasababu hujavaa Hijaab na unavutia. 
Mwanamke ambae havai Hijaab bila shaka anakusanya madhambi mengi, kwa sababu, wanaume wana nyoyo zenye matamanio na macho yenye kutaka. Hebu fikiria madhambi kiasi gani anayakusanya mwanamke huyu. Je, yale mema yote yanamtosha yakilinganishwa na madhambi yake? Fikiria akitoka, ndani ya mabasi, ndani ya treni, kazini, barabarani, na kila pahali, madhambi mangapi atapata kwa kila mwanamume anaemuangalia uzuri wake akamtamani?
Allaah Hakukuamrisha uvae Hijaab? Nakuogopea kuwa mema yako yana anguka kutoka kwenye mfuko uliopasuka. Yale mema yanaingia kwa juu na kutoka kwa chini. 
3.    MADAI YA KUZIDIWA NA JOTO
Mwanamke anaweza akalalamika kuwa nywele zake zinadondoka akivaa Hijaab kwa ajili ya joto, na akakuuliza, “unataka niwe kipara sasa?” Ewe dada, Allaah anasema kuwa moto wa jahannam ni mkali kuliko moto wa duniani. Mtume amesema: “Moto umezungukwa na matamanio yetu, na pepo imezungukwa na juhudi zetu.” Bado unaona tabu kuvaa Hijaab, unaona tabu kufuata maamrisho ya Allaah. 
4.   SI HOJA KUVAA HIJAAB KUWA NDIO HESHIMA
Wengine husema kuwa wanajua wanawake ambao wanavaa Hijaab lakini wana tabia mbaya kabisa. Kwa hivyo hawataki kuvaa Hijaab wakaonekana kama hao.Sasa basi kwa yule mwanamke anaedai  hayo:  Tunajua watu tele wanaoswali lakini wanafanya maaswia, hiyo   inamaanisha sisi pia tusiswali? Wengine ni mahujaji na wanafanya mambo yasiokuwa mazuri, je hii inamaana tusende hajj? Kwa hivyo dada yangu Hijaab sio mbaya, bali mwenye kuivaa na kuiharibia sifa zake ndio mbaya.
5.   ALLAAH HAJANIONGOZA BADO
Nitavaa Hijaab baadae lakini sio sasa kwa sababu Allaah hajaniongoza  bado. Kwa hivyo nikifika miaka hamsini baada ya   kufaidi ujana wangu, ndio nitavaa Hijaab. La, dada yangu! Hayo  ni makosa kabisa. Allaah anasema kuwa Habadili hali ya   watu mpaka wale watu  wabadili yaliyomo nyoyoni mwao. Huwezi kuvaa  Hijaab mpaka ujitahidi. Haikubaliki kusema kuwa Allaah hajakuongoza, la, Allaah amekuongoza kiasi ya kuwa unasoma makala haya. Sibabu ya wewe kusoma haya ni kuwa Allaah anakufungulia njia ya kuongoka, Nae Hamuachi mja Wake isipokuwa Anamuonesha uongofu, sasa ni   juu ya yule mja kufuata au kukanusha.
6.   NIKIOLEWA NDIPO NITAVAA HIJAAB.
Wanaume wengi wanapotaka kuoa, hutafuta wanawake wacha Mungu walio na heshima wanaovaa Hijaab. Munapotaka kuolewa, oleweni na     wanaume ambao watakupendeni kwa ajili ya dini yenu na watakao waheshimu. Kwa hivyo Allaah Atakupeni waume  walioshika dini. Yuko mtu alikwenda kwa ulamaa akamuuliza, “nikitaka kumuozesha   dada yangu, nimuozeshe mtu aina gani?” ‘Aalim akamjibu, “Muozeshe mwanamume ambae ni rafiki wa Uislamu, hivyo basi,   akimpenda, atamheshimu, na akimchukia hatomfanyia ubaya.  Kwa hivyo dada zangu, oleweni na wanaume ambao watakao wakinga na kuwaheshimu na kufurahikia kuwa nyinyi ni Muhjaba.

7.   MIMI BADO KIJANA
Unajua lini utaiaga hii dunia dada yangu? Vifo vya vijana vimeenea! Nitawapa mfano. Kisa hichi kilitendeka kikweli huko Misri (Egypt, Alexandria) wakati wa mwezi wa Ramadhani. Yuko mtu na mkewe ambaye ni mwenye kuvaa Hijaabu au muhajaba na majirani zao ambao ndani yake yumo msichana ambae hakuwa mwenye kuvaa Hijaab au  muhajaba. Huyo msichana   kama wasichana wengi wa Kiislamu alikuwa na moyo mzuri, lakini hakufahamu maana ya Hijaab katika Uislamu. Huyo mwanamke muhajaba alikuwa na uhusiano mzuri na yule msichana. Hakumpuuza kwa ajili havai Hijaab, la, alikuwa rafiki yake. Siku moja yule msichana alimuomba yule mwanamke ampeleke madukani akanunue jeans. Yule mwanamke muhajaba alikuwa na hikma na alijua kuwa ni lazima ampe yule msichana mawaidha, basi akakubali kumpeleka lakini kwa shuruti moja. Akamwambia amfuate kwenye muhadhara. Basi yule msichana akakubali. Walipokwenda kwenye muhadhara, mada ilikuwa kuhusu kutubia kwa Allaah. Basi yule msichana aliingiwa na imani nyingi kwa yale yaliyokuwa yakisemwa, mpaka akaanza kulia na huku akirudia maneno haya; ”nimetubu Mola wangu, nifunikeni”. Wale waliohudhuria wakamwambia watampeleka nyumbani ili akavae   Hijaab, lakini yule msichana alikataa, alitaka avae Hijaab pale pale,   akasema hawezi kutoka hapo bila ya kuvaa Hijaab. Basi akatafutiwa Hijaab akavishwa, akitoka tu na kutaka kudakia barabara, gari likamgonga, hapo hapo akafariki. Maasha Allaah! Msichana huyo alikufa baada tu ya kutubia, Subhana Allaah! Kwa hivyo wasichana, musitoe  sababu ya kuwa bado nyinyi ni wadogo, hakuna anaejua ataondoka  duniani saa ngapi.
8.   NATAKA KUFUATA FESHENI, NIKIVAA HIJAAB NITAACHWA NYUMA
Mola wako mlezi sio bora kuliko fasheni? Nakuhakikishia, ukivaa   Hijaab utakuwa  una nuru itokayo kwake.
9.   NATAKA KUIGA WATU WA MAGHARIBI (WESTERNERS).
Nani anaemheshimu mwanamke zaidi? Uislamu au wale ambao hawawezi kuuza kitu bila ya kuweka picha ya mwanamke aliye kuwa tupu? Wao ndio wamempa mwanamke heshima au wamemdhulumu? Au Uislamu uliomheshimu mwanamke na kumpa daraja za juu na   kumstiri kutokana na kudhulumiwa?
10.        SITAKI KUVAA HIJAAB KWA SABABU NAOGOPA NITAIVUA
Subhaana Allaah! Dada, kwanini huvai Hijaab na nia madhubuti huku unamuomba Allaah Akuhifadhi na kuitoa. Kuitoa Hijaab ni madhambi makubwa, usifanye hivyo, utakuwa unatoa mfano gani? Vaa Hijaab kisha ufanye mambo haya ili uhakikishe kuwa hutoitoa   Hijaab yako. 
1.          Kuwa na marafiki wema walioshika dini.
2.          Hudhuria na sikiliza mawaidha ya Kiislamu.
3.          Omba dua kwa Allaah Akuzidishie Imani ya dini yako na Akupe guvu ili uvae Hijaab yako kila siku.
11.        KUONA HAYA
Naona haya na aibu kutokana na yale watakayoyasema marafiki zangu nikivaa Hijaab. Dada, hutaona haya mbele ya Allaah siku ya kiama? Hutotahayuri mbele ya Mtume Muhammad? Hakuna kutahayari wala kuona haya mbele ya waja ikiwa unamuasi Mola wako.
Siku ya kiama utakuwa na kiu cha ajabu, na Mtume atakuwa anawapa watu maji. Utamkimbilia Mtume ili na wewe upate maji, lakini Malaika wawili watakuzuia ili usimfikie Mtume. Nae Mtume atawaambia wale Malaika wakuache kwasababu wewe ni katika umma wake. Wale Malaika watamwambia Mtume kuwa huyu ni katika wale ambao hawakufuata maamrisho ya Allaah. Basi Mtume ataondoka na kwenda mbali nawe huku anasema hataki uhusiano wowote na wewe kwa ajili hukufuata maamrisho ya Allaah.
Nani atatahayari wakati huo? Yule ambae anaonesha mapambo yake kwa kila mtu au yule anaejistiri na kujiheshimu?  Mtume amesema: “Ukamateni Uislamu na mikono yenu na meno yenu”.
Nawasisitiza dada zangu katika Uislamu, mukitaka kuvaa Hijaab, vaeni sasa musisubiri     baadae, kwani hamujui kama mutafika wakati huo munaoutarajia. Ukivaa Hijaab sasa, Mshukuru Allaah, swali kwa saa zake, tafuta marafiki wema na soma Qur-aan kila siku hata kama ni kidogo.
Mukifanya mambo hayo, basi inshaAllaah Hijaab yako itakwenda sambamba na kuabudu kwako, tabia yako njema, na pia utakuwa mfano mzuri kwa wanawake Waislamu na wasiokuwa Waislamu. 
Ukiwa umeamua kuwa muhajaba, basi usifikirie kuwa kuvaa Hijaab ndio kumekamilisha ibada zako na utaingia peponi, la, kuvaa Hijaab ndio miongoni mwa njia za kuelekea kwa Allaah.     
Kumbuka kuwa wewe ni mfano kwa wanawake Waislamu na wasiokuwa Waislamu, kwa tabia yako njema, kuabudu kwako, mavazi yako, na kadhalika. Bila shaka utamuathiri kila anayekuona hata bila ya kusema chochote. Utakuwa umeisafisha jamii, na matendo yako mema yako katika daraja ya juu mbele ya Allaah. Utawaongoza dada zako katika Uislamu kwasababu wewe ndio mfano na waziri wa Waislamu. 
Yafuatayo ni machache tu kuhusu namna ya kuvaa Hijaab. Ikiwa hufuati haya, basi ina maana kuwa huvai Hijaab sawa sawa.
1.   Sio lazima uvae Khimaar au ‘Abaayah. Unaweza ukavaa chochote, alimradi iwe ndefu na sio ya kushika mwili, na ifunike mwili wote. Ukivaa chochote ambacho kinaonesha umbile la miguu, kiuno, mabega, kifua, na kadhalika, basi hujavaa Hijaab sawa sawa.
2.   Kutovaa nguo nyembamba zinazoonyesha mwili.
3.   Kujifunika mwili mzima.
4.   Kutovaa nguo zinazofanana na nguo za kiume.
5.   Kutotia manukato unapotoka nje.
6.   Ukifuata hoja hizi wakati wote, basi umekamilisha Hijaab na umekuwa Muhajjabah In shaa Allaah.
EWE DADA YANGU KATIKA UISLAMU HIJABU NI VAZI MAALUMU LENYE SIFA MAALUMU.
WABILLAH TAWFIIQ
IMEKUSANYWA NA NDUGU YENU KATIKA UISLAMU: TAWAKKAL JUMA HUSSEIN KUTOKA KATIKA KITIVO CHA SHERIA NA SHARI’AH CHUO KIKUU CHA WAISLAMU-MOROGORO. USISITE KUULIZA UKITAKA UFAFANUZI ZAIDI. NAMBA YANGU YA SIMU NI +255 717 32 60 55.