Thursday, November 17, 2011

SALAMU ZA NDOA SEHEMU YA (II)

Kila sifa njema ni  zake Allah (s.w.t) muumba wa viumbe wote. Rehema za mwenyezi Mungu zishuke kwa Mtume Muhammadi (s.a.w) na watu wake wote.
TALAKA ni halali lakini ni halali inayochukiza kwa mwenyezi Mungu kwa sababu ya maudhi na madhara yanayo patikana baada ya wanandoa kutengana. Juu ya hii Mtume (s.a.w) anasema “ JAMBO  LA HALALI KULIFANYA LAKINI LINACHUKIZA SANA MBELE YA MWENYEZI MUNGU (S.W.T) NI MTU KUTOA TALAKA (Yaani kumuacha mke)”
Watu wanapokuwa katika ndoa wajue kuwa wako katika vazi, rehema, upendo na amani, lakini wanapoachana mambo hayo yote hutoweka na kusababisha matatizo na maudhi na pengine hujiingiza katika  maovu, na kama walibahatika kupata watoto basi watakosa malezi ya wazazi wote kwa pamoja na hivyo kuwafanya wakose kujengewa msingi mzuri wa KIMAADILI.
Katika uislamu hatuna mafunzo yanayo wafanya watu watengane, bali mafunzo tuliyonayo ni yakuwasuluhisha watu wapatane, na jambo hili ni jukumu la kila aliye kiongozi kuhakikisha kuwa anawapatanisha watu  waliogombana. Mwanamke anaweza kupewa talaka kama atafanya makosa makubwa yaliyowazi, kuwa muasi katika dini au kwa sababu yeyote ya msingi ya kisheria. Lakini hatua hii iwe ni hatua ya mwisho baada ya kutanguliwa na hatua zingine za awali za upatanishi.
Waliowengi miongoni mwetu wanafikiri kuwa talaka ni lazima tu iandikwe kwenye karatasi. Talaka inaweza kuandikwa, katika karatasi au inaweza kutolewa kwa matamko tu kama vile, nimekuacha, uko huru, ondoka tu , si mke wangu n.k. itaswihi maadamu tu yametolewa maneno hayo kwa nia ya talaka.    
Talaka inawahusu wale walio funga ndoa kisheria. Ifahamike kuwa mtu asiandike au kuzungumza jambo la talaka akasema ati nilikiwa ninatania, utani wake hautakubaliwa kisheria.
Mume anaruhusiwa kumiliki talaka tatu (3) lakini cha ajabu ni kwamba utamuona mtu anamtolea mkewe talaka zaidi ya tatu (3) huo sio uislamu bali ni USHETANI. Na hairuhusiwi kuzitoa talaka kwa  pamoja, bali talaka hutolewa moja moja. Na talaka ya kwanza na yapili huitwa talaka REJEA, yaani mume anaruhusiwa kumjerea mke wake ndani ya EDA yake. Na kama EDA yake ikiisha hana ruhusa kumrejea bali kwa ndoa nyengine tena akitaka. Na talaka ya tatu inaitwa talaka ya BAYANA, na mwenye kumpa mke talaka tatu hana ruhusa ya kumrejea mpaka aolewe na mume mwingine na sheria hapa inasema mpaka afanye naye tendo la ndoa halafu amuache kisha akae EDA amalize ndipo atapata ruhusa ya kumuoa tena kama anataka.
EDA zimegawanyika namna mbili yaani eda ya mwanamke kufiwa na mumewe na EDA ya talaka. EDA ya mwanamke aliyefiwa na mume wake kama ni mjamzito basi EDA itaisha mara atakapojifungua na kama si mjamzito atakaa  kwa muda wa miezi minne (4) na siku kumi (10) na mwanamke mwenye kukaa EDA kwa ajili ya kupewa talaka  kama ni mjamzito naye EDA yake itaisha mara tu baada ya kujifungua  na kama hana ujauzito basi atakaa kwa muda wa miezi mitatu. Mwanamke aliyepewa talaka moja  ndiye anayezungumziwa hapa.
Mwanamke mwenye kukaa EDA asitolewe hapo katika nyumba na wala hana ruhusa ya kutoka mwenyewe isipokuwa  akileta mambo ya ouvu yaliyo wazi inaruhusiwa kumfukuza. Mke anapokaa EDA basi ni jukumu la mume kumpa huduma huyo mke aliyempa talaka, vilevile ni jukumu la jamaa wa mume kumhudumia  mke aliyefiwa na mume wake mpaka EDA itakapoisha.
Huduma inayozungumziwa hapa ni ile ya mahitaji ya msingi na wala siyo kufanya naye ZINAA.
Ama watu wengi wanauliza ati, kwa nini mke akae EDA na mume asikae EDA? Kwa kifupi ni kwamba mume ndiye mchunga wa mke kwa hiyo muda wa mke ambao anakaa EDA ni kumpa nafasi ajiangalie hali yake kama  anaujauzito au la vilevile kwa upande wa EDA ya talaka inakuwa ni nafasi ya kuwafanya waliotengana kuombana msamaha na hivyo kufungua ukurasa mpya.
Ewe Mwenyezi Mungu nakuomba umuongoze kila anayesoma ujumbe huu na umruzuku kila anayesambaza ujumbe huu na vilevile uwape nguvu na moyo waislamu wengine kufanya kazi kama hii angalau kutoa mwongozo au ukumbusho kwa wengine. Mungu akiendelea kuniwezesha kwa hali na mali sitachoka daima nanyi wasomaji naomba mniombee mafanikio katika kazi hii INSHAALAAH. 

No comments:

Post a Comment