Thursday, November 17, 2011

KILA MUISLAMU ANADHIMA YA KUENDELEZA UISALAMU.

Shukrani  zilizo takasika ni zake Allah (s.w.t) asiyekuwa na mshirika katika  Ibada yake  wala katika  ufalme  wake.
Rehema na Amani zishuke juu ya Mtume Muhammad (s.a.w) na wale wote wenye kushikamana naye.
Mwenyezi Mungu ametujaalia wanadamu kuwa makundi mbali mbali  kama vile  masikini  na  matajiri, wafanyakazi  na  wakulima  na  makundi  mengine  mengi. Pamoja na  kuwepo na  makundi  mbali mbali  kila  kundi  linatakiwa  kumcha  Allah (s.w.t) na kuwa mstari wa  mbele  katika  kuendeleza  dini.
Wewe na mimi  tumetamka shahada mbili  na tumekiri katika nyoyo zetu kuwa mwenye jina la Allah ndiye  Mungu wa  kweli  na Muhammad ni Mtume wake, Kukiri na kutamka shahada ni dalili tu ya kujulisha  kuwa sisi ni waislamu. Ili uislamu wetu uweze kukamilika  tunatakiwa  kuyafanya  yale ambayo wametuagiza Allah (s.w.t.) na Mtume wake (s.a.w) na kuyaacha yale ambayo wametukakaza.
Katika  makundi tuliyonayo wanadamu,  kundi la wafanya kazi huwa wamepitia  hatua mbalimbali kama vile shule ya msingi, sekondari, chuoni na  hatimaye kazini. Sasa ewe uliyejaaliwa kuajiriwa ujiulize  ukiwa shule  ya  msingi, sekondari na chuoni, mlianza wangapi, mlifaulu  wangapi na mpaka hivi sasa ni wangapi mnaendelea na kazi?
Je, wale ambao hawakufanikiwa katika yale maeneo ambayo wewe umefanikiwa unafikiri ni uzembe wao  au Allah hakuwawezesha? Na wewe uliyefanikiwa unafikiri umefanikiwa kwa ujanja wako au Allah ndiye aliyekuwezesha?
Allah (s.w.t) humpa amtakaye na humnyima amtakaye, umekuwa miongoni mwa waliopewa na Allah basi nawe utoe katika njia ya Allah ili kuendeleza dini yake si kwaajili ya kumnufaisha mwenyezi mungu bali ni kwaajili ya kutaka radhi ili aendelee kukuruzuku na kulinda  mali  yako.
Mwenyezi Mungu anatuhimiza kwa kusema ndani ya Quran: ENYI MLIOAMINI TOENI KATIKA VILE TULIVYOKUPENI KABLA HAIJAFIKA SIKU AMBAYO HAPATAKUWA (NA) KUJIKOMBOA WALA URAFIKI (WA KUSAIDIANA) WALA UOMBEZI, NA WALIOKUFURU NDIO WALIO JIDHULUMU (KWELIKWELI) Q:2:254.    
Allah (s.w.t.) ametuumba wanadamu akatupa uwezo kuliko viumbe wote, ametupa elimu, akatupa pia uhuru wa kuweza kupanga na kupangua,  kutanda na  kutandua, kufunga  na kufungua  na mengine  mengi.  Tujiulize  enyi wenzangu, katika kipato  chetu  tunatumia kiasi  gani  katika  mambo  ya anasa?
Kwanini tunakunja mikono yetu katika upande wa kundeleza dini yetu?
Sisi tuliojaaliwa kuwa na uhakika wa kipato  tena kwa muda maalumu tunakuwa wazito kutoa. Je, wale wasio kuwa na uhakika wa kipato kwa muda maalumu wataweza? Waislamu wenyewe tusipo iendeleza dini yetu asiye kuwa Muislamu ataweza kuundeleza Uislamu?
Allah (s.w.t) amemsifu binaadamu kwa kusema “ HAKIKA TUMEMUUMBA MWANAADAMU KATIKA UMBO LILILO BORA KABISA”Q 95:4. Hapa inamaana wewe na mimi tumejaliwa  vipawa  vinavyoweza kutuwezesha kutambua dhima ya kuumbwa kwetu na hatima ya maisha yetu hapa duniani na kesho akhera.
Enyi ndugu zangu katika imani na dinI  tujitahidi kutoa bila kuwa na mashaka ya kulipwa katika vile tunavyovitoa, Allah  ameahidi kumlipa kila  mtu kwa kila akifanyacho kiwe cha  kheri au shari, kidogo au kikubwa, akiwa ametoa kwa siri au wazi kama  anavyosema ndani ya Quran 2:274 “WALE WANAOTOA MALI  ZAO USIKU NA MCHANA KWA SIRI NA DHAHIRI, WANAUJIRA WAO KWA MOLA WAO, WALA HAITAKUWA KHOFU JUU YAO  WALA HAWATAHUZUNIKA”
Ewe Mwenyezi Mungu , kila atakaye kunjua  mkono wake na kutoa kwako basi mtengenezee mambo yake hapa Duniani na Kesho Akhera.

No comments:

Post a Comment